Jumapili, 23 Juni 2019



NJIA
PENYE NIA PANA NJIA,PANA NJIA SIYO NDIYO NIA.
Kati ya kazi ngumu inayotushinda na kutupelekea vijana wengi wenye ndoto na malengo makubwa kuishia njiani ni katika maandalizi ya uundaji wa njia bora kwa ajili ya watu watakaotufuata nyuma yetu.
Yabebe malengo yako kama sululu, ibebe ndoto yako kama beleshi na yaambatanishe maono yako kama jembe, Vaa mabuti ya ujasiri na jiveshe glavu za uthubutu kisha kachimbe na kuiunda vema njia yako.

VIJAMBO VIUNDAVYO NJIA KUU NA NJEMA
Nina vijambo kadha kwa siku ya leo katika kusaidiana kwenye ujenzi wa njia na upanuzi wa kile tunachokipigania katika maisha yetu.
 
JAMBO LA KWANZA
Ili iwezekane kwetu kuiunda njia ni lazima tuibebe imani ndani yetu hata kama itakuwa ni kubwa kuliko umri wetu na nzito kuliko uzito wetu lazima tukubali tu kuibeba.
Imani zetu hupotea pale pahala unapofikia wakati wa kila mmoja wetu akionekana ana mtoto na siye hatuna,kila mmoja wetu ana mke na siye hatujui hata mahari yalipwaje,kila mmoja wetu anaonesha kuanza kufanikiwa nasi twazidi kuparamiwa na hasara na kufirisika hata kabla ya kutajirika, ule wakati siye ni mahoehae na twaonekana mazube kwa kuamini mitazamo chanya yetu huku wengine wakifanikiwa haraka haraka kupitia waganga,kamari,kubashiri na kuuza hata visivyo halali.
Hizo ndizo nyakati ambazo vijana wengi huziacha njia zetu na kwenda kuzijaribu njia za mkato ili tu tusionekane tumeshindwa huku tungekuwa na imani kuu ndani yetu tungeamini kwamba kushindwa ni sehemu ya kujifunza tu na tungeendelea na kuunda njia zetu.
JAMBO LA PILI
Tunapokwama ni pale magumu yanapokuwa yamesongamana njiani kiasi cha kushindwa kuona mbele.
Ni ngumu kumwambia mtu aliyekata tamaa asikate tamaa huku tayari tamaa alikwisha anza nayo awali kabla hajaanza kuikata.
Vijana wengi tupo hivyo huwa tunaanza kwa kuwa na tamaa kubwa katika uundaji wa njia kisha ikianza kukatika nasi twakatika katika na kusawajika kabisa kiasi cha kushindwa kuokoteka maana tayari msongo na mfadhaiko vinakuwa vimeshauvaa uhuru na amani yetu.
Nataka ninene na ngoma zako za pina kisha nipenye katika pinea yako ili usisahau kirahisi kwamba:-
Karibisha kila kitu katika maisha yako ila hakikisha unakaribisha vya msingi pekee katika fikra zako ili uwe imara katika kupambana na hofu maana kuna pahala utapachimba na kuinuka na nyoka na pahala bee utapachimba litainuka jiwe na kukuumiza hiyo haitamaanisha utupe zana na uache kuiunda njia
JAMBO LA TATU
Epusha kabisa ubwabwajaji ovyo katika uundaji wa njia yako.
Hakuna wawili katika kuunda njia moja tambua njia yako ni yako tu na yake ni yake tu.
Kinachotukwamisha wengi ni kuwashwa kusemasema mambo yetu kwa kila mmoja hata kwa wale walioshindwa kuziunda njia zao unategemea utapata nini kama sio kubezwa,kukejeliwa, kukatishwa tamaa na hata kupingwa.
Jifunze sana kuiunda njia yako katika ukimya kiasi cha kuepusha hata zana zako zisigongane pindi uchimbapo kuiunda vema njia yako.
Ibebe sana imani ya Mwenyezi Mungu ndani yako katika kuiunda njia yako maana ulimwengu wa sasa una mengi hasa ukionesha una mengi ya kuyafanya.
Kumbuka katika kitabu Yohana 14 mstari na aya ya 6 maandiko yanasema
Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
No photo description available.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni